Polisi wamewakamata washukiwa watatu zaidi wanaohusishwa na sakata ya utoaji kazi ghushi iliyogunduliwa na Makachero wa idara ya DCI wiki mbili zilizopita.
Kulingana na mkurugenzi wa DCI George Kinoti, mamia ya watu wanaotafuta kazi wanaaminika kupoteza zaidi ya milioni 200 katika ulaghai huo, baada ya kuahidiwa kazi katika mashirika mbalimbali ya serikali, ikijumuisha vitengo muhimu vya kiusalama vya serikali.
Washukiwa wawili walikamatwa siku ya ijumaa. Senior Sergent Jackson Mureithi Manyara na corporal Zachary Kimathi Cosmas, ni maafisa wa magereza Wanaoaminika kuwa walisajiliwa na mshukiwa mkuu Grace Nyamohanga, jukumu lao likiwa kupokea pesa kwa ajili ya kazi hizo hewa.
Mshukiwa wa tatu Peter Ngare Githu, ambaye makaazi yake yako eneo la juja kaunti ya Nairobi, anaamika kusajili watu 50 na kukusanya milioni 16 kutoka kwao.
Watatu hao wanatarajiwa kuwasilishwa mahakamani siku ya jumatatu pamoja na Grace Nyamohanga na Masiaga Slvester, kwa ajili ya kusomewa mashtaka.