Makachero kutoka idara ya upelekezi ya DCI siku ya Ijumaa walimkamata Irene Njoki Irungu kwa madai ya kuwalaghai wateja katika kumbi za starehe kwa kuwawekea dawa katika vinywaji vyao katika Kaunti ya Kiambu na vitongoji vyake.
Kulingana na ripoti ya polisi iliyotolewa muda mfupi baada ya kukamatwa kwake na kuzuiliwa, Mshukiwa alijibandika jina la Mitchelle ili kulinda utambulisho wake.
Katika kile kilichogundulika na makachero wa DCI kama uwepo wa mzunguko wa genge la wahalifu linaloendesha biashara hiyo, Mshukiwa na msaidizi wake Peter Irungu, ambaye pia yuko mikononi mwa polisi, wanashirikiana kunyemelea wateja na kuwawekea dawa katika vinywaji vyao na baadaye kuwaibia.
Kulingana na Makachero , dawa wanayoitumia kuwalaghai wateja huwafanya waathiriwa kupoteza fahamu kwa zaidi ya saa kumi na mbili, jambo linalowapa fursa kutekeleza wizi wao na kutoroka bila ya kukamatwa.