Marufuku ya kitaifa ya watu kutotoka nje kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri imeongezwa kwa siku sitini zaidi.
Kupitia notisi ya sheria nambari 89, Waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang'i amesema kuwa agizo hilo litatekelezwa katika maeneo yote ya jamhuri ya taifa la Kenya.
Agizo hilo lilianza kutekelezwa tarehe 28 Mei 2021 na litaendelea kwa kipindi cha siku sitini.
Serikali aidha imekataza mikusanyiko ya umma , matembezi ya mtu mmoja mmoja au makundi nyakati za kafyu, isipokuwa kwa idhini kupitia njia ya maandishi , itakayotolewa na afisa wa polisi anayehudumu katika kaunti au eneobunge.